Exodus 17:8-16

Vita Na Waamaleki

8 aWaamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu. 9 bMose akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”

10 cKwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Mose alivyomwagiza, nao Mose, Aroni na Huri wakapanda juu ya kilima. 11 dIkawa wakati wote Mose alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda. 12 eMikono ya Mose ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Aroni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Mose, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti mpaka jua lilipozama. 13Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.

14 fKisha Bwana akamwambia Mose, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”

15 gMose akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisi.
Yehova Nisi maana yake ni Bwana ni Bendera yangu.
16 iMose akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa mpaka kwenye kiti cha enzi cha Bwana. Bwana atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kutoka kizazi hata kizazi.”

Copyright information for SwhNEN